MHE. KANGI LUGOLA AZINDUA OPERESHENI YA USAFI

Harakati mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuweka Majiji, halmashauri na miji, yetu safi,  ikiwa ni pamoja na matamko mbalimbali ya viongozi wakuu hapa nchini. Aidha, Halmashauri za miji na majiji zimekuwa zikiendesha kampeni za usafi kwa kuweka siku maalumu za kufanya usafi wa mazingira na pia kusimamia sheria, kanuni, miongozo na sheria ndogo izinayohusu mazingira.

Nguvu za ziada zinahitajika ili halmashauri kuchukua hatua za dhati za kudhibiti taka pamoja na kuhakikisha sheria ndogo na sheria nyingine zinatekelezwa kwa vitendo ili kuhakikisha usafi wa mazingira unasimamiwa ipasanyo na kuhakikisha mazingira yanayotuzunguka yanakuwa masafi.
Pamoja na kuwepo kwa sheria mbalimbali bado usafi wa mazingira hauridhishi, taka ngumu katika maeneo mbalimbali kama maeneo ya makazi na maeneo ya biashara hazizolewi kwa wakati, utunzaji wa mifereji ya maji ya mvua na utunzaji wa bustani za burudani haujafikia kiwango kinachostahili, taka bado zinatupwa ovyo kando kando ya barabara na chini ya madaraja na pia taka kutumika kama njia ya kuziba makorongo na kuzuia mmomonyoko wa kingo za mito katika makazi ya watu. Tabia hii imesababisha kuziba kwa mifareji iliyotengenezwa kwa gharama kubwa wakati wa mvua na kusababisha mafuriko ambayo yamepelekea nyumba nyingi kujaa maji na kuharibu mali za wananchi na hata kusababisha vifo.